Mashambulizi ya anga yaliushambulia mji mkuu wa Sudan siku ya Jumamosi huku mapigano yakiingia wiki yake ya nne saa chache kabla ya pande zinazohasimiana kukutana nchini Saudi Arabia kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana.
Mamia ya watu wameuawa tangu kuibuka kwa mzozo huo hapo April 15 kati ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na msaidizi wake aliyegeuka kuwa mpinzani mkuu Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).
Mapigano hayo yameshuhudia ndege za kivita zikilenga mabomu mjini Khartoum na vikosi viwili vya majenerali wanaohasimiana vikishiriki katika mapigano makali ya mitaani katika mji huo wenye wakaazi milioni tano. Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano yalifikiwa lakini hakuna hata mmoja yaliyoheshimiwa.
Katika taarifa ya pamoja, Marekani na Saudi Arabia wanasema jeshi na vikosi vya RSF watafanya mazungumzo ya moja kwa moja Jumamosi mjini Jeddah, wakielezea kama mazungumzo ya awali ya mashauriano.