Marekani imetangaza kwamba inatoa dola milioni 83 za ziada katika msaada wa dharura kwa wakimbizi wanaokimbia mapigano huko Sudan Kusini.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilieleza kuwa mgogoro huko Sudan Kusini unatishia kusababisha njaa na inaeleza kuwa zaidi ya watu milioni mbili tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.
Taarifa inaeleza kuwa tangu mapigano ya hivi karibuni yalipoanza mwezi Disemba kuna zaidi ya wakimbizi wapya 450,000. Ilielezea kwamba idadi hiyo ni kubwa kuliko ile idadi ya ile ya wakimbizi walioathirika mwaka 2005 wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini kumaliza vita vvya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan kati ya upande wa kaskazini na kusini.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilieleza kwamba msaada mpya wa fedha utatumiwa kwa ajili ya chakula, huduma za afya, mbegu na vifa vya kulima na kufanya jumla ya msaada kwa Sudan Kusini mwaka huu kufikia zaidi ya dola milioni 720.
Ghasia hizo mpya huko Sudan Kusini zilianza na mzozo wa kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na naibu wake wa zamani Riek Machar. Mapigano ya kikabila kati ya majeshi yanayounga mkono serikali na yale yanayoiunga uwasi yamesababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kuwa 10,000 na kusababisha zaidi ya wa-Sudan Kusini milioni moja kukimbia kutoka kwenye nyumba zao tangu mwezi Disemba.