Marekani kutoa hadi dola milioni 250 zaidi, zikiwa msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Kasha la silaha kutoka Marekani likipakiwa kwelekea Ukraine. Picha ya maktaba.

Marekani itatoa hadi dola milioni 250 zaidi, zikiwa msaada wa kijeshi kwa Ukraine, ambao unajumuisha roketi za kurusha makombora ya HIMARS na AIM-9M Sidewinders, yanayoweza kutumika kulinda anga ya taifa hilo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kutoa silaha za Sidewinders kwa Ukraine, ambazo zinaweza kutumika kwa masafa mafupi kwenye mashambulizi ya anga kwa anga.

Msaada huo pia unajumuisha vifaa vya kuondoa vilipuzi vya kuzikwa ardhini, pamoja na silaha za kujilinda dhidi ya vifaru, kwa mfano TOW, pamoja na makombora ya kurusha kutoka mabegani. Msaada huo ni wa 45 kuidhinishwa na Rais kutoka kwa wizara ya ulinzi ya Marekani, tangu Russia ilipofanya uvamizi wa Ukraine Februari 2022.

Hata hivyo silaha za masafa marefu kama zile za ATACMS, hazijawekwa kwenye msaada huo suala ambalo limezua ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wachambuzi kama vile Liuteni Jenerali mstaafu Ben Hodges aliyekuwa kamanda wa jeshi la Marekani barani Ulaya, kati ya 2014, na 2017.