Mapigano yazuka katika baadhi ya maeneo ya Sudan katika siku ya 100 ya vita

Moshi ukifuka katika eneo la kusini mwa jiji la Khartoum tarehe 29 Mei 2023, Picha na AFP.

Mapigano yalizuka katika baadhi ya maeneo ya Sudan katika siku ya 100 ya vita siku ya Jumapili huku majaribio ya upatanishi wa kieneo na kimataifa wa mataifa yenye  nguvu yameshindwa kutafuta njia ya kutoka katika mzozo unaozidi kuwa mgumu.

Mapigano hayo yalianza Aprili 15 wakati jeshi na kikosi cha RSF walipoanza kugombea madaraka. Tangu wakati huo zaidi ya watu milioni 3 wamekimbia ikiwa ni pamoja na zaidi ya 700,000 ambao wamekimbilia katika nchi jirani.

Takriban watu 1,136 wameuwawa kwa mujibu wa wizara ya afya ingawa maafisa wanaamini kuwa idadi ni kubwa zaidi.

Si jeshi wala kikosi cha RSF kimeweza kutangaza ushindi huku vikosi vya RSF vikidhibiti mapigano ya ardhini katika mji mkuu Khartoum dhidi ya vikosi vya anga na mizinga ya jeshi.

Miundo mbinu na serikali katika mji mkuu imesambaratika huku mapigano yakienea upande wa magharibi hasa katika smkoa tete wa Darfur na pia kusini ambako kundi la waasi la SPLM-N limejaribu kuchukua eneo.