Mapigano kati ya majenerali wanaohasimiana wa Sudan katika jimbo la Darfur siku ya Jumapili yamesababisha vifo vya raia wasiopungua 12, amesema daktari mmoja katika eneo hilo lililoharibiwa.
Akizungumza kutoka mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, daktari huyo alisema mapigano yamesababisha raia 12 kuuawa katika eneo la Nyala. Lakini chanzo hicho kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama kilieleza kwamba vurugu za mapigano zinazuia harakati za waathirika kwenda hospitalini.
Wakaazi wa mji huo waliripoti kuwepo mapigano siku ya Jumamosi, kwa mashambulizi ya risasi na makombora katika eneo la Nyala. Darfur, eneo kubwa la magharibi kwenye mpaka na Chad, limeshuhudia ghasia mbaya zaidi katika mapambano ya kuwania madaraka kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani, kamanda wa wanamgambo wa Rapid Support Forces, Mohamed Hamdan Daglo.
Umoja wa Mataifa unasema ghasia katika jimbo la Darfur zimechukua mwelekeo wa kikabila na huenda zikachukuliwa kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.