Je Unajua : Mambo muhimu yanayohusu Kombe la Dunia?

Mandhari ya mapambo yaliyoko katika nchi ya Russia kabla ya kuanza Kombe la Dunia

Wakati washabiki wa michuano ya Kombe la Dunia 2018 wakiwa tayari kushuhudia weledi wa timu mbalimbali katika mashindano haya, bila shaka wengi wanajiuliza ni vitu au mambo gani yalio tofauti katika michuano ya mwaka huu ukilinganisha na Kombe la Dunia 2014. Baadhi ya mambo huenda unayajua lakini :

Je Unajua?

1.Mchezaji yupi aliye na umri mdogo kuliko wote: Jumla ya wachezaji 736 watashirikifainali za kombe la dunia huko Russia kuanzia Juni 14. Daniel Arzani wa Ufaransa ndiye aliye na umri mdogo kuliko wote. Alizaliwa Januari 4, 1999, hivi sasa akiwa na miaka 19. Mfalme wa kandanda duniani Pele wa Brazil, alicheza katika fainali ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17.

2.Mchezaji aliye na umri mkubwa: Golikipa wa timu ya taifa ya Misri, El Hadary ana umri wa miaka 45. El Hadary ambaye ni kipa wa klabu ya Pharao ya misri, anaichezea timu hiyo tangu mwaka 1996. Ni mara yake ya kwanza kushiriki kombe la dunia. El Hadary anavunja rikodi ya Faryd Mondragon, aliyekua mlinda mlango wa timu ya Colombia katika kombe la dunia la mwaka 2014, akiwa na umri wa miaka 43. Hadary anavunja pia rikodi ya mchezaji mwengine mkongwe, ambae ni Roger Milla aliyeichezea timu ya taifa ya Cameroon katika kombe la dunia la mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka 42.

3.Mchezaji mwenye uzoefu wa kombe la dunia: Mchezaji aliye na uzoefu zaidi wa kombe la dunia ni Rafael Marquez wa timu ya taifa ya Mexico. Marquez, ambaye ni beki wa kati, anashiriki kombe la dunia kwa mara ya tano akiwa na umri wa miaka 39.

4.Timu ya taifa yenye wachezaji walio na umri mdogo: Timu ya Ufaransa ndiyo ina wachezaji walio na umri mdogo. Wastani wa umri wa wachezaji ni miaka 26, wachezaji wa timu hiyo wanalingana kiumri na wachezaji wa Super Eagles ya Nigeria. Baadae inafuatiwa na timu ya taifa ya Spain ambayo wastani wa umri wa wachezaji ni miaka 27.

5.Timu ya taifa yenye wachezaji walionunuliwa kwa pesa nyingi: Timu ya ufaransa ndiyo kwa ujumla wachezaji wake walinunuliwa kwa pesa nyingi katika klabu zao kuliko timu nyingine. Wachezaji hao walinunuliwa kwa zaidi ya Euro billioni moja, timu inayofuata ni Spain.

6.Mchezaji mrefu kuliko wengine: Mchezaji mrefu kuliko wengine, ni golikipa wa timu ya Croatia Lovre Kalinic mwenye urefu wa futi 6 na inchi 6 . Anayefuata ni goli kipa wa timu ya Ubelgiji Thibaut Courtois anaye ichezea pia timu ya Chelsea, ambaye ana urefu wa futi 6 na inchi 5.

7.Mchezaji mfupi kuliko wengine: Ni mchezaji wa timu ya taifa ya Panama Alberto Quintero, mwenye urefu wa futi 5 na inchi 4.

8.Timu yenye jezi bora kuliko zingine:Super Eagles ya Nigeria.

9.Timu ambayo imeshiriki kombe la dunia kuliko zingine: Timu ya Brazil imeshiriki fainali za kombe la dunia mara nyingi kuliko timu zingine. Imeshiriki mara 20, Ujerumani inakuja nafasi ya pili kwa kushiriki mara 18.