Malawi imepiga marufuku uingizaji wa mahindi kutoka Kenya na Tanzania kutokana na wasiwasi wa kuenea kwa ugonjwa wa Mahindi Lethal Necrosis ambao kunaweza kuharibu chakula kikuu kinachotegemewa huko. Zaidi ya watu milioni 4 katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Afrika wanakabiliwa na uhaba wa chakula.
Kenya na Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa vyanzo vikuu vya mahindi kwa Malawi wakati wa vipindi vya uhaba wa chakula.
Hata hivyo, Wizara ya Kilimo ya Malawi ilitangaza marufuku wiki hii ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje katika taarifa inayosema ugonjwa wa Mahindi unaosababishwa na Lethal Necrosis hauna tiba na unaweza kusababisha hasara ya mavuno kwa asilimia 100.
Taarifa hiyo inasema Mahindi yanaweza tu kuingizwa nchini mara tu yanaposindikwa, ama kama unga au mbegu.
Henry Kamkwamba ni mtaalamu wa kilimo katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Sera ya Chakula. Ameiambia VOA kuwa marufuku hiyo itaisaidia Malawi kujikinga na ugonjwa huo.
“Kama mnavyofahamu baadhi ya mbegu tayari zimeharibika kutokana na ukame wa muda mrefu na watu wanapanda kwa mara ya pili. Tukiagiza baadhi ya mahindi haya, kuna uwezekano kwamba baadhi ya mahindi ambayo yataingizwa nchini, yanaweza kutumika kama mbegu ingawa hayajapendekezwa kama mbegu”.
Kamkwamba anasema mara ugonjwa huo ukiingia nchini itakuwa vigumu kuudhibiti.“Fikiria jinsi tulivyopoteza ndizi zetu zote siku za nyuma na sasa Malawi ni muagizaji wa ndizi kwa sababu ya masuala fulani yanayotokana na sera zetu zisizo makini katika suala la uagizaji. Tuliishia kuagiza virusi vilivyojaa kwenye ndizi. Na kuna wasiwasi kama huu kutokea kwenye mahindi”.
Malawi inakabiliwa na uhaba wa chakula, kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za kimbunga Freddy kilichopita mwezi Machi, ambacho kiliharibu maelfu ya hekari za mahindi, zao kuu la chakula nchini humo.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani nchini Malawi na Kamati yaTathmini ya Athari Malawi wanakadiria kuwa watu milioni 4.4, karibu robo ya idadi ya watu nchini humo, watakabiliwa na uhaba wa chakula hadi Machi mwaka ujao.
Grace Mijiga Mhango, ni Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Nafaka nchini Malawi. Anasema kuwa wakati anaelewa ukubwa wa athari za ugonjwa wa mahindi, kupiga marufuku uagizaji wa mahindi wakati tupo kwenye uhitaji kunaweza kusababisha kupanda kwa bei.
“Kama kweli hatuna chakula cha kutosha basi tunabuni ongezeko jingine la mahindi lisilo la lazima kwa sababu mbadala wa kuagiza mahindi lazima iwe Afrika Kusini. Na Afrika Kusini ni mbali sana na hawana ya kutosha. Ikimaanisha, tukipata bidhaa kutoka Afrika Kusini, itakuwa ghali”.
Serikali ya Malawi inasema marufuku hiyo itakuwa ya muda huku ikichunguza hatua nyingine za kujikinga kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo.