Mahitaji ya usalama ya Ukraine, ya haraka na ya muda mrefu yanatarajiwa kutawala kwenye majadiliano wakati mawaziri wa ulinzi wa NATO watakapokutana Alhamisi na Ijumaa huko Brussels mahala ambapo Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Reznikov atawafahamisha washiriki juu ya maendeleo ya vita vya Ukraine dhidi ya Russia.
Dharura ya mahitaji hayo, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar aliiambia VOA katika mahojiano ya Jumatano, ni silaha kwa nchi yake kulinda anga zake dhidi ya mashambulizi ya angani ya Russia na kuendeleza jitihada zake za muda mrefu za kukamata tena baadhi ya maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na Russia zoezi ambalo lilianza wiki iliyopita.
Ombi la muda mrefu la Kyiv ni kwa ajili ya kuingia mapema kwenye muungano wa kujihami wa mataifa 30, ombi ambalo linaonekana kupewa uzito wa kusikilizwa kwa makini wakati wakuu wa nchi za NATO watakapokutana mwezi ujao huko Vilnius, Lithuania. Wiki hii, mawaziri wanatarajiwa kutathmini upya mahitaji ya kijeshi ya Ukraine, kuratibu ushirikiano, na kukagua uwezo wa ulinzi wa muungano huo.
Nchi wanachama pia zinajadili baadhi ya hatua za uanachama kamili wa NATO ambazo zinaweza kukamilishwa huko Brussels. Katika mahojiano yake, Maliar alisema vikosi vya Ukraine vinasonga mbele, hatua kwa hatua, mashariki na kusini mwa nchi hiyo na vimechukua tena kilomita za mraba 90 za eneo tangu kuanza kwa mapigano.