Mahakama ya Russia ilimkuta na hatia mkosoaji wa Kremlin Alexei Navalny ya ubadhirifu na dharau siku ya Jumanne, hatua ambayo inaelekea kupelekea muda ambao mkosoaji huyo mkubwa wa Rais Vladimir Putin ataokakaa gerezani ukiongezeka kwa miaka kadhaa.
Navalny tayari anatumikia kifungo cha miaka miwili na nusu katika gereza moja mashariki mwa Moscow kwa ukiukaji wa msamaha unaohusiana na mashtaka ambayo anasema yalitungwa ili kuzuia matakwa yake ya kisiasa.
Katika kesi ya hivi punde ya jinai inayomkabili, ambayo pia ameitaja kama ina ushawishi wa kisiasa, anaweza kuongezewa hadi miaka 13 jela katika kifungo hicho.
Navalny akionekana amedhoofika kimwili alisimama kando ya mawakili wake kwenye chumba kilichojaa maafisa wa usalama wa magereza huku hakimu akisoma tuhuma dhidi yake. Navalny mwenye umri wa miaka 45 alionekana kutoshtuka, akitazama chini huku akipitia nyaraka za mahakama.