Mahakama moja ya Afrika Kusini Jumatatu ilianza kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma juu ya kifungo chake kirefu gerezani kufuatia maandamano makali dhidi ya kufungwa kwake.
Kulingana na Reuters, mawakili wa Zuma waliomba mahakama kumwachilia huru Zuma mwenye umri wa miaka 79 kwa sehemu kwa sababu kwa madai kwamba mahakama ya Katiba ilitoa hukumu hiyo isivyo sawa wakati hayupo.
Zuma aliripoti kwenye kituo cha magereza katika mkoa wake wa Kwa Zulu-Natal wiki iliyopita kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 kwa mashitaka ya kudharau mahakama baada ya kushindwa kutoa ushahidi mbele ya uchunguzi maalum ukiangalia tuhuma mbali mbali za ufisadi wakati wa miaka yake tisa madarakani ambayo ilimalizika mnamo mwaka 2018. Mawakili wake pia wanasema kuwa atakuwa katika hatari ya kuambukizwa COVID-19 wakati akiwa gerezani.
Zuma amekanusha madai hayo na kukataa kushiriki katika uchunguzi ambao ulianza wakati wa wiki zake za mwisho madarakani.