Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Ijumaa, jopo la majaji watatu wa Rufaa limeondoa amri hiyo iliyowekwa Juni 30, wakati rufaa iliyowasilishwa na waziri Ndung’u ikisubiriwa.
Awali Ndung’u kupitia kwa mwanasheria mkuu wa Kenya, Justin Muturi aliwasilisha rufaa mahakamani akisema kwamba serikali huenda ikapoteza takriban shilingi bilioni 211, ndani ya mwaka huu wa kifedha iwapo sheria hiyo itasitishwa.
Waziri huyo alisema kwamba bila kutekelezwa kwa sheria hiyo, serikali ya Kenya Kwanza haitaweza kutekeleza majukumu yake ya bajeti ya mwaka 2023/24 kama ilivyopangwa. Majaji Mohammed Warsame, Kathurima M’Inoti na Hellen Omondi wamesema kwamba mswada wa fedha una siku 90 kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa kifedha.