Maelfu ya wakazi wa Argentina Jumanne wamemiminika kwenye barabara za mji mkuu wa Buenos Aires, ili kuishangilia timu yao iliyochukua kombe la dunia ikiongozwa na nyota Lionel Messi.
Umati mkubwa wa watu ulielezewa kuwa ulisimamisha msafara uliokuwa na basi la wachezaji wa timu hiyo. Wachezaji wasingeweza kufika kwenye sanamu ya Obelisco katikati ya mji kama ilivyopangwa kutokana na sababu za kiusalama.
Vyombo vya habari vya ndani vilikadiria kwamba takriban watu milioni 4 walikusanyika mjini humo. Wachezaji walilazimika kuhamishwa kutoka kwenye basi lao kwa kutumia helikopta.
Matias Gomez ambaye ni fundi vyuma mwenye umri wa miaka 25 amesema kwamba sherehe hizo ni mojawapo ya matukio muhimu zaidi kushuhudiwa katika maisha ya mwanadamu.