Maelfu wakusanyika katika nchi kadhaa kulaani ukamataji wa watu wanaoandamana Iran

Waandamanaji wakiwa wameshikilia mabango nje ya Ubalozi wa Iran mjini London, Jumapili, Septemba 25, 2022. Wakipinga kifo cha Muirani Mahsa Amini, aliyefariki nchini Iran akiwa chini ya ulinzi wa polisi (Picha ya AP/Ruzuku ya Alastair).

Maelfu ya watu walikusanyika katika nchi kadhaa duniani siku ya Jumapili kulaani Ukamataji wa watu  wanaoandamana nchini Iran  maandamano ambayo yalianza baada ya kifo cha msichana mdogo wakati akiwa chini  ya ulinzi wa polisi.

Maelfu ya raia wa Iran walijitokeza barabarani katika muda wa wiki mbili zilizopita kupinga kifo cha Mahsa Amini, msichana mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikamatwa na polisi wa maadili wa Iran katika mji mkuu wa Tehran kwa madai ya kutofuata masharti ya mavazi ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Familia yake ilidai kuwa alipigwa, huku maafisa wakidai alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.

Takriban watu 92 wameuwawa katika msako huo, shirika lenye makao yake nchini Norway la Iran la Haki za Kibinadamu -IHR lilisema Jumapili. Shirika hilo pia lilisema kumekuwa na uzuiaji mkubwa wa watu kupata mtandao.

Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa takriban waandamanaji 41 na polisi wameuawawa tangu maandamano hayo yaanze Septemba 17.

Ripoti ya shirika la habari la Associated Press ya taarifa rasmi za mamlaka ilithibitisha kuwa takriban watu 14 wameuawa, huku zaidi ya waandamanaji 1,500 wakikamatwa.