Machungaji mashuhuri wa Uganda alazwa hospitalini baada ya shambulizi la risasi

Polisi wa Uganda mjini Kampala kwenye picha ya maktaba.

Mchungaji mashuhuri wa Uganda na ambaye pia ni muungaji mkono sugu wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, amelazwa hospitali baada ya shambulizi la bunduki ambalo lilimuuwa mlinzi wake, polisi wamesema Jumatano.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mchungaji Aloysius Bugingo alipigwa risasi Jumanne jioni baada ya watu wasiojulikana kushambulia gari lake, na kisha kutoroka kwa kutumia pikipiki mjini Kampala, ripoti imeongeza.

Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa kiume wa Museveni na ambaye huenda akawa mrithi wa baba yake, amesema kwamba alizungumza na “mfuasi wao sugu” Bugingo, na kwamba yupo sawa. “Alipata majeruhi madogo kwenye bega lake la kushoto,” ameongeza kusema kupitia ukurasa wake wa X, akilitaja tukio hilo kuwa la “kikatili.’

Bugingo ni mmoja wa watu mashuhuri wenye utata nchini Uganda, akiwa kiongozi wa kanisa la House of Prayer Ministries, likiwa moja wapo ya makanisa ya kipentekoste, lenye ushawishi mkubwa zaidi kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki. Pia anamiliki vituo vya televisheni na radio, ambavyo huwa akivitumia kumuunga mkono Museveni ambaye ametawala Uganda tangu 1986.