Maandalizi ya Kombe la Dunia ya Morocco yamegubikwa na utata wa makocha

Emerick wa Gabon akipiga shuti na kufunga dhidi ya Morocco wakati wa mechi yao ya Kombe la Mataifa ya Afrika mjini Libreville.

Maandalizi ya timu ya taifa ya Morocco - Simba wa Atlas katika michuano ya Kombe la Dunia yamegubikwa na utata kuhusu kocha wao  huku wakikabiliwa na kibarua kizito wakitaka kurudia mafanikio yao ya mwaka 1986 walipokuwa taifa la kwanza la Afrika kutinga katika raundi ya pili.

Morocco ilimfukuza kazi Vahid Halilhodzic mwezi Agosti, miezi michache kabla ya fainali hizo, baada ya mzozo wa muda mrefu kati ya kocha huyo wa Bosnia na rais wa chama cha soka Morocco -FA kuhusu uteuzi wa wachezaji.

Mwaka jana, Halilhodzic aliwafukuza winga wa Chelsea, Hakim Ziyech na mlinzi wa Bayern Munich, Noussair Mazraoui kwa sababu za kinidhamu na alikataa wito wa mkuu wa chama cha soka Fouzi Lekjaa kuwarejesha kwenye kikosi.

Halilhodzic alifutwa kazi na chama cha soka nchini humo ambacho kilimteua mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Morocco Walid Regragui kama mrithi wake baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika ngazi ya klabu.

Regragui, 47, aliwarudisha Ziyech na Mazraoui katika kikosi chake cha kwanza na wawili hao walianza mechi za kirafiki dhidi ya Chile na Paraguay mwezi Septemba.

“Hakim Ziyech amerejea kwenye timu ya taifa kwa sababu anastahili. Unapoona jinsi Hakim anavyocheza, unajiambia mwenyewe ni vigumu kutomchezesha kwenye Kombe la Dunia ,” alisema Regragui.

Kocha huyo alishinda taji la ligi nchini Qatar akiwa na Duhail mwaka 2020 kabla ya kuiongoza Wydad Casablanca ya Morocco kwenye ligi ya nyumbani na Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mwaka huu.

Morocco haijafuzu hatua ya makundi tangu ifikie raundi ya pili mwaka 1986 nchini Mexico na wako katika kundi gumu linalojumuisha timu inayoshika nafasi ya pili duniani Ubelgiji na timu ya Croatia waliomaliza katika nafasi ya pili kwenye Kombe la Dunia 2018 pamoja na kuimarika kwa kasi kwa timu ya Canada.

"Najua maandalizi ya Kombe la Dunia yalikuwa mafupi ... Tutapambana kuwafurahisha mashabiki wa Morocco," Regragui alisema baada ya kuteuliwa mapema mwezi Septemba.

Wanatumai kushinda matarajio na kujipatia angalau pointi moja kutoka kwenye kila mechi kati ya mechi mbili za kwanza kabla ya kukabiliana na Canada katika mechi ambayo inaweza kuwakilisha nafasi yao nzuri ya kuandikisha ushindi wao wa kwanza kwenye fainali hizo tangu mwaka 1998. Je wataweza?