Maafisa Pakistan wanasema shambulio la waasi liliua wanajeshi 12 na raia mmoja

Shambuliio la waasi dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Pakistan

Vyombo vya habari vya jeshi vimesema kuwa “magaidi” watano walijaribu “kuingia katika kituo hicho”, katika wilaya ya kaskazini ya Zhob mapema asubuhi, lakini wanajeshi waliwazingira

Maafisa nchini Pakistan wamesema Jumatano kuwa shambulio la waasi dhidi ya kambi ya kijeshi na mapigano katika maeneo mengine katika jimbo la Baluchistan, kusini magharibi mwa Pakistan liliwaua wanajeshi 12 na raia mmoja.

Vyombo vya habari vya jeshi vimesema kuwa “magaidi” watano walijaribu “kuingia katika kituo hicho”, katika wilaya ya kaskazini ya Zhob mapema asubuhi, lakini wanajeshi waliwazingira.

Makabiliano hayo yaliyodumu saa kadhaa yaliwaua wanajeshi tisa na washambuliaji wote, taarifa ya jeshi imesema. Haikutoa maelezo zaidi, lakini vyanzo vya kuaminika vya usalama huko Zhob viliripoti wanajeshi wasiopungua 12 pia walijeruhiwa na walitarajia idadi ya vifo kuongezeka.

“Vikosi vya usalama na taifa linaendelea kuwa imara na wamedhamiria kuzuia majaribio yote ya adui, yenye lengo la kuharibu amani ya Baluchistan na Pakistan,” jeshi limesema katika taarifa yake.

Afisa wa ngazi ya juu wa utawala kwenye eneo, hapo awali alithibitisha kuwa wanamgambo walivamia eneo la Zhob. Azeem Kakar aliwaambia waandishi wa habari kwamba raia walinaswa katika majibizano ya risasi na kusababisha mwanamke mmoja kufariki na watu watano kujeruhiwa.