Jeshi la Polisi nchini Tanzania limekiri kuwashikilia maofisa 12 waliokamatwa kufuatia uchunguzi unaofanywa na wataalamu waliobobea katika uchunguzi wa makosa ya uhalifu wa kifedha wa jeshi hilo, kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa dhidi ya wahusika wa wizi wa makontena 329 katika bandari ya Dar Es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam siku ya Jumatatu, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai- CP, Diwani Athuman aliwataja watuhumiwa watano wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni na Tiagi Masamaki, ambaye ni Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Habib Mponezia, ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Huduma za Ushuru na Eliachi Herieli Mrema, Msimamizi Mkuu wa ICD - Azam.
Your browser doesn’t support HTML5
Wengine ni Haroun Mpande wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT - TRA na Khamis Ally Omary ambaye ni Mchambuzi Mwandamizi wa masuala ya Biashara TRA.
Hata hivyo mkurugenzi huyo wa makosa ya Jinai hakuwataja watuhumiwa wengine saba wanaoshikiliwa na jeshi hilo kutokana na sababu za upelelezi, ambapo alisema wanatarajia kukamilisha uchunguzi mapema iwezekanavyo na kuwafikisha mahakamani mara moja.
Novemba 27 mwaka huu, Waziri Mkuu bwana Majaliwa Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi ya kushtukiza katika bandari ya Dar Es Salaam ambapo aliibua kashfa hiyo ya wizi wa makontena na ukwepaji wa kodi wa takribani shilingi za kitanzania bilioni 80.