Mashindano ya mpira wa miguu ya nchi za Ulaya “Euro 2016” yanaanza Ijumaa Juni 10 2016 mjini Paris, Ufaransa huku washabiki wakiwa na shauku kubwa sana ya kujua nani atakayeweza kutwaa taji hili kwa mwaka huu. Mashindano haya ya mwaka huu yanaonekana kama yanaweza kuwashangaza mashabiki wa soka kwa sababu kuna timu nyingi ambazo hazikupewa nafasi kubwa kwenye hatua za awali za mtoano lakini zimeonyesha uwezo mkubwa sana wa kusakata kabumbu.
Mabingwa watetezi Hispania pamoja na wenyeji Ufaransa wanapewa nafasi kubwa sana kutwaa taji hili, lakini kuna timu kama Ujerumani, Ubelgiji na Croatia ambazo zina uwezo mkubwa zinaweza kufanya yasiyotarajiwa kwenye mashindano haya.
Mabingwa wa dunia Ujerumani watawakosa nyota wake wa kutegemewa kutokana na kuumia, Antonio Rudiger, Marco Reus na Ilkay Gundogan, wakati beki wake wa kutegemewa Matts Hummels anatarajiwa kukosa mechi mbili za mwanzo kutokana na kuumia.
Kikosi chipukizi cha Ubelgiji ambacho kimekuwa kinatabiriwa kufanya mambo makubwa kwenye soka kina nyota wengi ambao ndio kwanza wamepona kutoka kwenye kuumia kama Thibaut Courtois, Jan Vertoghen na Kevin De Bruyne na wengine wamekuwa na msimu mbaya na timu zao kama nyota wa kutegemewa anayechezea timu ya Chelsea ya Uingereza, Eden Hazard.
Uingereza ikiwa na chipukizi walio na matumaini makubwa lakini mabeki wasio makini sana haipewi nafasi kubwa na wachambuzi wa soka.
Ureno ikiwa na mwanasoka nyota wa dunia Cristiano Ronaldo, inapewa nafasi kubwa zaidi huku kikosi chao kikiwa na mchanganyiko wa wachezaji chipukizi na wachezaji wakongwe. Hii ni nafasi nzuri kwa Cristiano Ronaldo kuonyesha uwezo wake mkubwa akiwa na timu yake ya Taifa.
Ufaransa ndio inayopewa nafasi kubwa zaidi ukizingatia kuwa mashindano haya yanachezewa nyumbani na wameshafika hatua ya robo fainali mara mbili kwenye mashindano mawili yaliyopita huku kikosi chao kikiwa na viungo chipukizi na mahiri kabisa barani Ulaya kama Paul Pogba na Antoine Griezmann.