Korea Kusini ilituma kwa ghafla angani ndege zake za kijeshi baada ya ndege za kijeshi za China na Russia kuingia ndani ya mpaka wake wa ulinzi wa anga (ADIZ) kusini na mashariki mwa Peninsula ya Korea siku ya Jumanne, tukio ambalo lilifuatia matukio mawili ya hivi karibuni ya kukaribiana kwa ndege za Marekani na China katika Mlango Bahari wa Taiwan na Bahari ya Kusini mwa China.
Wizara ya Ulinzi ya China imesema katika taarifa yake kwamba ndege hizo zilizoingia ndani ya mipaka yake ya ulinzi ADIZ ya Seoul zilikuwa zikishiriki katika mazoezi ya pamoja ya anga na Russia katika bahari ya Japan na East China Sea, ikiwa ni zoezi la sita tangu mwaka 2019.
Mazoezi ya hivi karibuni yalizinduliwa baada ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Seoul. Eneo la ulinzi wa anga la Korea Kusini, ADIZ sio sehemu ya anga ya nchi nzima; Hata hivyo hakuna nchi iliyotoa taarifa kwamba ndege zake zilikuwa zinaingia katika eneo hilo, kulingana na shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini.