Vyombo vya habari vya serikali vilimuonyesha Kim, akiwa amevalia koti la ngozi, akichungulia nje ya dirisha la jengo la uchunguzi wakati kombora hilo likinyanyuliwa na kutoka kwenye bomba la moto Alhamis, kwenye njia ya kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pyongyang.
Katika ripoti ya Ijumaa asubuhi, shirika la habari linalomilikiwa na serikali la Korea (KCNA) lilisema jaribio la kombora aina ya Hwasong-17 ni sehemu ya juhudi za kuimarisha kizuizi cha vita vya nyuklia cha Korea Kaskazini.
Silaha mpya ya kimkakati ya DPRK itaonyesha wazi uwezo wa kikosi chetu cha kimkakati kwa dunia nzima kwa mara nyingine tena, Kim alinukuliwa akisema akitumia kifupi cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, jina rasmi la Korea kaskazini.
Hili ni jaribio la nne la ICBM kwa Korea kaskazini na la kwanza tangu mwaka 2017 wakati wa kilele cha mvutano kati ya Kim na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Mwaka 2018 Kim alitangaza kusitishwa kwa majaribio ya makombora ya masafa marefu, lakini alianza tena uzinduzi wa masafa mafupi hapo mwaka 2019.