Kiongozi wa Taliban auawa Pakistan

Hakimullah Mehsud kiongozi wa Taliban aliyeuawa Novemba 1, 2013

Maafisa wa Pakistan wanasema kuuawa kwa kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Taliban Hakimullah Mehsud katika shambulizi la ndege ya Marekani isiyoongozwa na rubani (drone),huenda kukadhoofisha mazungumzo ya amani na kundi hilo.

Maafisa wa Marekani na wale wa Pakistan wanasema Mehsud aliuawa Ijumaa wakati makombora manne ya ndege za CIA yalipogonga uwanja wake kaskazini mwa mkoa wa Waziristan. Wakati wa mazishi yake leo Jumamosi ndege hizo zisizotumia rubani zilikuwa zimepaa katika eneo alilozikwa. Mashahidi wanasema baadhi ya wafuasi wake walijaribu kuzifyatulia risasi wakiwa wamejawa na hasira.

Kulikuwa na habari za kutatanisha kwamba kundi hilo la Taliban limemchagua kiongozi mpya. Baadhi yao wanasema Khan Said Sajna ambaye alikuwa wa pili katika uongozi wa Taliban amepanda cheo kuongoza kundi hilo leo Jumamosi. Lakini wengine walimnukulu msemaji wa Taliban akisema uamuzi huo hujafikiwa na kwamba kiongozi mpya atatangazwa katika siku za karibuni.

Mehsud mwenye umri wa miaka 34 alianza kuongoza kundi hilo mwaka wa 2009 baada ya kiongozi aliyemtangulia kuuawa. Marekani ilikuwa imetangaza zawadi ya dola milioni 5 kwa yeyote atakayesaidia kukamatwa au kuuawa kwa Mehsud.

Alikabiliwa na mashataka ya kutekeleza shambulizi la mhanga wa kujitolea kwenye uwanja wa idara ya kijasusi ya Marekani CIA nchini Afghanistan mwaka wa 2009 na shambulizi lililoshindikana la bomu katika eneo la Times Square jijini NewYork mwaka wa 2010.