Kampuni ya Maikha yafanya onyesho la mavazi Elkridge Maryland

Bi. Maimuna Kivugo kati kati akiwa na wasichana wenzake warembo waliovaa mavazi ya kampuni yake ya Maikh.

Maimuna amekulia katika familia ya wapishi na mafundi wa nguo na anasema babu yake ndiye aliyemfanya apende tasnia hiyo ya mavazi

Jamii ya watanzania wanaoishi washington Dc na vitongoji vyake walishuhudia maonyesho ya pili ya mavazi ya kampuni ya MAIKHA katika mji wa Elkridge katika jimbo la Maryland nje kidogo ya jiji la Washington.

Kampuni ambayo inamilikiwa na kijana anayeishi Marekani Maimuna Kivugo ambaye ni mmiliki aliandaa maonyesho hayo.

Dipping in Sheen ndio kauli mbiu iliyotamalaki usiku huo katika ukumbi wa Best Western Hotel Elkridge Md , ambapo mmiliki wa kampuni ya Maikha na kijana mwenye umri wa miaka 25 Maimuna Kivugo ambaye ni mwanafunzi wa uhandisi wa ujenzi na uchoraji ramani katika chuo kikuu cha Hartford amesema lengo kuu la kuandaa onyesho hilo la mavazi ni kuonyesha umahiri wake katika fani nyingine ambayo ni fasheni.

Maimuna amekulia katika familia ya wapishi na mafundi wa nguo na anasema babu yake ndiye aliyemfanya apende tasnia hiyo ya mavazi.

Suala la mavazi limepewa kipaumbele cha kipekee na Maimuna akilenga wanawake kujipa uhuru zaidi na heshima, akisema nguo zilizotengenezwa na wasichana kwa ajili ya wasichana zinasheherekea urembo, nguvu ya mwanamke na aina tofauti.

Maimuna anasema ameingia katika mavazi akiwa analenga kuwasaidia wanawake wenzake kujisitiri na vile vile kupendeza hasa wale walio na imani ya dini ya kiislam na hawataki mavazi ya kuvunja imani yao.

Wakazi wa DMV yaani vitongoji vya Washington Dc, Md na Va walijitokeza kushuhudia maonyesho hayo na kuvutiwa kwa namna ya pekee na vijana hao katika kazi yao.

Maimuna anasema haya hayakuja kirahisi kwani amepitia changamoto nyingi lakini hakukata tamaa. Akiwataka vijana wenzake wasimame imara katika kutimiza ndoto zao.

Kwa ujumla kampuni hii inamilikiwa na kijana na anafanya shughuli zote na vijana wenzake katika jiji hili na vitongoji vyake na wameweka mfano bora kwamba vijana wanaweza kufanikisha wakiamua ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kutoka kwa wazazi wao na kuonyesha si lazima wakae na kungoja mikopo au misaada ya kifedha.

Imetayarishwa na Sunday Shomari.