Wapiganaji watatu zaidi waliuawa katika shambulio la Israel lililomuua jenerali mwandamizi wa jeshi la Iran, la Revolutionary Guards karibu na mji mkuu wa Syria, limesema shirika linalofuatilia vita.
Shambulio hilo la Jumatatu lilimlenga Razi Moussavi, kamanda mwandamizi wa cheo cha juu, katika kikosi cha Quds, tawi la kigeni la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC), aliyeuawa nje ya Iran katika kipindi cha karibu miaka minne. “Wapiganaji wawili wa kigeni na mpiganaji mmoja raia wa Syria pia waliuawa katika shambulio la Israel,” limesema shirika linalofuatilia vita, la Syrian Observatory for Human Rights.
Moussavi alilengwa muda mfupi baada ya kuingia katika shamba kwenye eneo linalodhibitiwa na makundi yanayoungwa mkono na Iran, lilisema shirika hilo lenye makao yake Uingereza, ambalo lina mtandao mkubwa wa vyanzo katika eneo.
Wakaazi wa wilaya ya Sayyida Zeinab kusini mwa Damascus, ambako shambulio hilo lilitokea, waliripoti kuwa makundi yanayoungwa mkono na Iran yameimarisha usalama katika eneo hilo.