Tshisekedi ataka serikali ya Joseph Kabila isitambuliwe

Kiongozi wa upinzani nchini DRC, Etienne Tshisekedi.

Wafuatiliaji wa hali ya kisiasa wana wasiwasi kwamba hali ya machafuko iliyoko hivi sasa inaweza kulirejesha taifa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliuwa takriban mamilioni ya watu kati ya mwaka 1996 na 2003.

Kiongozi wa upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Etienne Tshisekedi amewataka watu wasiitambue serikali ya Rais Joseph kabila ambayo ipo madarakani kinyume cha sheria na si halali.

“Muda wake wa uongozi umeisha na yeye Kabila anaendelea kung’ang'ania madaraka na hakuna dalili za kuitisha uchaguzi,” alisistiza Tshisekedi siku ya Jumanne.

Lakini Mahakama mmoja nchini DRC imetoa uamuzi kwamba Kabila anaweza kuendelea kushikilia madaraka mpaka pale uchaguzi utakapoitishwa.

Pia Chama kinacho tawala kimependekeza uchaguzi ufanyike Aprili 2018.

Katika video iliyobandikwa kwenye mtandao wa You Tube, Tshisekedi aliwasihi watu kujibu kwa amani, kile alichosema mapinduzi ya kijeshi yaliyoungwa mkono na mahakama ya katiba.

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa wakazi katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa DRC, Kinshasa, walipaza sauti usiku wa manane kutoa ishara kwamba ni wakati wa Kabila kuondoka madarakani.

Milio ya risasi pia ilisikika katika wilaya kadhaa. Mshauri wa rais, Barnabe Kikaya alisema ilikuwa ni kinyume cha katiba kusema kwamba Kabila aondoke madarakani haraka haraka.

Maandamano jana Jumatatu yalifanyika sehemu kadhaa mjini Kinshasa, licha ya amri iliyotolewa ikipiga marufuku maandamano na pia jeshi kutanda kila mahali.

Kwa mujibu wa mashuhuda polisi walifyatua gesi za kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji.

Wameongeza kuwa Sehemu kubwa ya mji mkuu haikuwa na watu huku maduka yakiwa yamefungwa na watu wakikaa majumbani kwa kuhofia ghasia.

Huko mashariki mwa DRA katika mji wa Goma makundi ya haki za binadamu yanasema darzeni ya waandamanaji walikamatwa.

Kabila amekuwa Rais wa DRC tangu baba yake alipouawa mwaka 2001. Alishinda chaguzi mbili mwaka 2006 na 2011 katika kile wapinzani wake walichokiita ni kuchakachuliwa kwa kura. Pia katiba inamzuia kugombea awamu ya tatu.

Congo haijawahi kuwa katika utulivu tokea ilipopata uhuru kutoka Ubelgiji katika miaka ya 60.

Wafuatiliaji wa hali ya kisiasa wana wasiwasi kwamba hali ya machafuko iliyoko hivi sasa inaweza kulirejesha taifa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliuwa takriban mamilioni ya watu kati yam waka 1996 na 2003.