Jenerali wa Sudan akataa pendekezo lililoongozwa na Kenya kuwa walinda amani wa Afrika Mashariki wasaidie kumaliza vita

Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan (kushoto), mjini Juba Oktoba 14, 2019 na Mohamed Hamdan Daglo (Kulia), ambaye anaongoza Kikosi cha RSF, wakihutubia wanahabari aliporejea kutoka Russia katika uwanja wa ndege wa Khartoum Machi 2, 2022. AFP

Jenerali mmoja wa Sudan akataa pendekezo lililoongozwa na Kenya kwamba walinda amani wa Afrika Mashariki wasaidie kumaliza vita vya zaidi ya siku 100 nchini Sudan

Jenerali mmoja wa Sudan alikataa akitoa lugha ya vitisho pendekezo lililoongozwa na Kenya kwamba walinda amani wa Afrika Mashariki wasaidie kumaliza vita vya zaidi ya siku 100 nchini Sudan katika video iliyotolewa Jumatatu na kukosolewa vikali na mamlaka ya Kenya.

Mapigano hayo ya Jeshi la Sudan na vikosi vya RSF yamepokea maombi mengi ya upatanishi wa kimataifa lakini hakuna waliofaulu kukomesha au hata kusitisha kwa kiasi kikubwa mapigano hayo yaliyozuka tangu Aprili 15

Mapema mwezi huu IGAD jumuiya ya kanda ya Afrika Mashariki ambayo Kenya ni mwanachama ilipendekeza mpango ambao utajumuisha kupelekwa kwa walinda amani katika mji mkuu Khartoum.

Jeshi la Sudan limekataa mara kwa mara mpango huo unaoongozwa na Kenya likishutumu mamlaka hiyo ya kikanda kuunga mkono vikosi vya RSF.