Jedwali la robo fainali Afcon lakamilika

Washabiki wa Senegal wakishangilia timu yao katika michuano ya AFCON huko Cameroon.

Washabiki wa Senegal wakishangilia timu yao katika michuano ya AFCON huko Cameroon.

Equatorial Guinea ilihitaji mikwaju ya penalti kuifungasha virago  Mali kwa mabao 6-5 baada ya sare ya 0-0 katika muda wa nyongeza, ili kutinga robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika la TotalEnergies, Cameroon 2021.

Vijana wa Nzalang Nacional walitinga robo fainali kwa mara ya tatu huku Mali wakishindwa kurudia kile walichokifanya Cameroon miaka 50 iliyopita walipotinga fainali mwaka 1972.

Golikipa wao Jesus Owono alikuwa shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penati ya Mali katika mechi hiyo iliyokuwa na mvutano wa hali ya juu.

Nao Misri wamefuzu kuingia robo kufuatia ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Ivory Coast.

Mafarao wa Misri walishinda kwa mikwaju ya penalti na kuwalaza Ivory Coast huku mlinda mlango wao wa akiba Mohamed Daader akiwa shujaa baada ya kuokoa mkwaju wa Eric Bailly.

Mechi hiyo ilitazamwa na umati wa watu wenye shauku kwenye Uwanja wa Japoma.

Kwa hiyo jedwali la Afcon robo fainali limekamilika ambapo wenyeji Cameroon tarehe 29 siku ya Jumamosi watacheza robo fainali na Gambia wakati Burkinafaso watapepetana na Tunisia.

Na tarehe 30 Misri watapambana na Morocco wakati Lions of Teranga Senegal watakwaana na Equatorial Guinea .