Ripoti zinasema kampeni kali sana zinafanyika wakati jeshi likitarajia kuingia mjini humo wakati wowote. Shirika la habari la AFP limesema kwamba mmoja wa wanahabari wake ameripoti kusikia mfululizo wa makombora kwenye miji ya Khan Younis na Rafah.
Mji wa Rafah uko karibu na mpaka wa Misri, ambako maelfu ya wapalestina walitafuta hifadhi kutokana na mapigano yanayoendelea. Ripoti zimeongeza kusema Irael imefanya mashambulizi ya anga kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat na katikati mwa Gaza na kuvunja maeneo mawili ya Hamas huko Beit Lahia kaskazini mwa Gaza.
Ripoti za mashambulizi kadhaa huko Gaza zimetolewa baada ya maafisa wa afya kusema kwamba karibu watu 200 wameuwawa ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita. Umoja wa Mataifa umeshutumu kile ilichokiita Israel hivi karibuni kuulenga msafara wa misaada wa magari ya misaada kwenda Gaza kulikofanywa na vikosi vya Israel.
Thomas White mkurugenzi wa shirika la UN, la UNRWA linaloshugulikia wakimbizi wa Palestina, alisema Ijumaa kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba wanajeshi wa Israel waliushambulia msafara wa magari ya misaada kaskazini mwa Gaza, kwenye njia ambayo ilitengwa na jeshi la Israel.