Israel yaanza mashambulizi mapya ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza

Picha iliyochukuliwa kutoka kusini mwa Israel ikionyesha mosi kutoka kwenye majengo yalioshambuliwa Jumatano na Israel kwenye Ukanda wa Gaza. Dedemba 27. 2023.

Vikosi vya Israel Jumatano vimefanya  mashambulizi mapya ya anga huko Ukanda wa Gaza, siku moja baada ya matamshi kutoka baadhi ya maafisa wa Israel kuhusu kupanua mapambano ya ardhini, kuzua wasi wasi kutoka Umoja wa Mataifa kuhusiana na usalama wa raia.

Mashambulizi ya Jumatano yamejumuisha operesheni za ardhini za Israel na mashambulizi ya anga huko Gaza City, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, ambako awali Israel ililenga kampeni yake ya kuliangamiza kundi la wanamgambo la Hamas.

Baada ya kuingia kusini katika eneo la Khan Younis, maafisa wa Israel wiki hii wameonyesha dalili za kuingia kati kati mwa Gaza, yakiwemo maeneo yenye kambi kadhaa za wakimbizi.

Wengi wa wakazi wa Gaza wamelazimika kuondoka makwao kutokana na mapigano, huku wengi wakisongamana kwenye makazi ambayo tayari yameelemewa, huku wengine wakijitahidi kuondoka kabisa kufuatia maonyo ya Israel ya kuchukua hatua za kijeshi.

Huduma za kibinadamu pia zimeathiriwa na ghasia hizo, na kupelekea uhaba wa chakula, maji na mafuta.