Wizara ya mambo ya nje ya Iran imetangaza kuwa itafungua tena afisi zake za kibalozi nchini Saudi Arabia wiki hii na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya miaka saba ya mfarakano, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti Jumatatu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Nasser Kanaani amesema afisi hizo ni, ubalozi wa Iran mjini Riyadh, ubalozi wake mdogo mjini Jeddah, na ofisi ya mwakilishi wa kudumu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, zote zitafunguliwa rasmi Jumanne na Jumatano.
Mwezi Machi, Iran na Saudi Arabia zilikubaliana kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia, kutokana na makubaliano yaliyosimamiwa na China, ambayo yanawakilisha mafanikio makubwa katika kanda hiyo.
Saudi Arabia ilivunja uhusiano na Iran mwaka 2016 baada ya waandamanaji kuvamia ofisi za kidiplomasia za Saudi Arabia mjini Tehran na mji wa kaskazini mashariki wa Mashhad wakati wa maandamano yaliyochochewa na mauaji ya kiongozi wa kidini maarufu wa Kishia, na wengine 46 katika taifa hilo la kifalme lenye utajiri wa mafuta.