Na BMJ Muriithi
Wawaniaji wa tikiti ya chama cha Demokratic nchini Marekani, Hillary Clinton na Bernie Sanders, walikabiliana vikali jana usiku katika mdahalo wao wa nane uliofanyika katika chuo kikuu cha Miami Dade, kilicho katika jimbo la Florida, na ambao ulipeperushwa moja kwa moja na mashirika ya habari ya Univision na CNN.
Bi Clinton, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani na Seneta Sanders anayewakilisha jimbo la Vermont, walijadili maswala nyeti kama vile uhamiaji, mfumo wa afya na kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba.
Swala la uhamiaji lilijadiliwa kwa kina, huku kila mmoja wa wanasiasa hao, ambao wanatafuta uungwaji mkono ili kuwakilisha chama chao wakati wa uchaguzi wa urais mwezi Novemba, akisema ako katika nafasi bora zaidi kumshinda muwaniaji wa tikiti ya chama cha republican, Donald Trump, ambaye ameendelea kuongoza katika majimbo kadhaa.
Clinton alidai kwamba rekodi ya Sanders ya kupiga kura kwenye seneti ilionyesha kuwa hakuunga mkono mpango wa kuwasaidia wahamiaji wasio halali kuendelea kuishi nchini Marekani.
“Tulikuwa na uunwaji mkono wa Warepublikan kwenye mswada ambao ungepata njia kwa wahamiaji hao kupata uraia. Rais Obama alikuwa tayari kuitia saini sheria hiyo kama ingepitishwa…mimi nililipiga kura kuiunga mkono, lakini Seneta Sanders aliipinga,” alisema Bi Clinton huku akishangiliwa na waliokuwa ukumbini, wengi wao wakiwa ni wa asili ya Latino.
Lakini Sanders alishikilia kwamba hakuwa na nia mbaya alipopinga mswada huo.
‘Kila mswada una mema na mabaya. Na kuna mambo ambayo sikuyapenda katika mswada huo. Ndiyo maana mimi nikakapiga kura ya kuupinga.
Clinton na Sanders wanang’ang’ania kura za jimbo la Florida ambalo lina wajumbe wengi wa chama ambao ni muhimu sana katika kuamua ni nani atapeperusha bendera ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba.
Mdahalo huo ulikuwa wao wa mwisho kabla ya zoezi la kupiga kura za awali litakalofanyika siku ya Jumanne kwenye majimbo kadhaa, likiwemo la Florida.