Mataifa ya Afrika yaombwa wasiwatese washukiwa wa ugaidi

Vikosi vya jeshi la Kenya vikitoa ulinzi wakati wa mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu ugaidi, kwenye kituo cha kimataifa cha mikutnao cha Kenyatta mjini Nairobi Septemba 2, 2014.

Wataalamu wa haki za binadamu kutoka mataifa 44 ya Afrika wamekosoa ongezeko la matumizi ya mateso dhidi ya washukiwa wa ugaidi utaratibu unaotumika wakiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Hii ni tabia ambayo mataifa mengi inakabiliana nayo dhidi ya ugaidi, jinsi wanavyowatendea washukiwa wa ugaidi wakiwa chini ya ulinzi ili kuweza kupata habari zaidi kuzima harakati zao.

Wataalamu wa haki za binadamu wakihitimisha mkutano wao wa siku tatu mjini Yaounde, Cameroon wamewasihi viongozi wa Afrika kujitahidi kulishughulikia suala hili ili kuhakikisha kwamba wanaheshimu viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Omar Bongo wa tume ya kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Gabon amesema mataifa yote ya Afrika yanayokabiliwa na vitishio vya ugaidi hawaheshimu misingi ya haki za binadamu, na si vyema washukiwa kukumbwa na mateso au ukatili mwingine, vitendo visivyo vya kibinadamu au kuwadhalilisha au kuwaadhibu.

Amesema mataifa ya Afrika ni vyema yaweke sera na sheria ambazo zinaheshimu haki za binadamu wakati zinapokabiliana na ugaidi kwasababu watu wengi wanaoteswa inabainika hawana hatia.

Katika miaka ya karibuni Afrika imeona ongezeko la ugaidi barani humo.

Watalaamu wa haki katika mkutano hawakuzitaja nchi ambazo ni mbaya zaidi katika rekodi ya haki za binadamu. Watalaamu wamekosoa sheria ambazo zimepitishwa mwaka jana nchini Cameroon na Chad, mataifa mawili ambayo yanaathiriwa na mashambulizi ya kundi la Boko Haram, ambapo wamependekeza adhabu ya kifo kwa watu watakaopatikana na hatia ya kutenda, kuwasaidia au kufadhili vitendo vya ugaidi.

Watalaamu wa haki pia wamesema katika baadhi ya mataifa ya Afrika jeshi linapokuwa na kazi ya kukabiliana na ugaidi huwatesa washukiwa na kuwatendea kinyama.

Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Namibia, John Walters amesema jeshi ni vyema lipewe mafunzo ya kuheshimu haki za binadamu wakati linapofanya shughuli zake.

“Kuzuia ni vyema zaidi kuliko kutibu. Ndiyo maana tunajaribu kusema maafisa polisi wetu wapewe mafunzo ili wafahamu mateso ni kitu gani, na kwamba matumizi ya mateso kupata habari yamepigwa marufuku kabisa,” ameongezea Bw. Walters.

Umoja wa Mataifa Desemba 10, 1984 ilipitisha azimio dhidi ya mateso na vitendo vingine vya kikatili, vya kinyama au udhalilishaji na kuweka kutokomeza kama moja ya lengo lake kuu.