Guterres aeleza wasiwasi wake kutokana na mzozo uliyopo Sudan

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Katibu mkuu wa Umoja Mataifa Antonio Guterres, Jumapili ameelezea wasi wasi wake kutokana na mzozo unaoendelea  nchini Sudan kati ya vikosi vya Rapid Support Forces, RSF, na jeshi la serikali.

Kiongozi huyo pia amelaani vikali vifo pamoja na majeruhi kwa wakazi, vikiwemo vitatu vya wafanyakazi wa shirika la Chakula Duniani WFP, huko Dafur Kaskazini, huku wengine wawili wakijeruhiwa vibaya. Ameongeza kwamba wahusika wote ni lazima wawajibishwe haraka iwezekanavyo bila kuchelewa.

Baadhi ya majengo ya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa kwenye eneo la Darfur yanaripotiwa kuharibiwa wakati wa mapambano, huku mengine yakiporwa. Guterres amezikumbusha pande zinazozozana kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa, pamoja na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wote wa UN na mashirika mengine ya kimataifa, pamoja na majengo yao.