Ghasia Mombasa baada ya Sheikh kuuawa

Mmoja wa walionusurika baada ya Sheikh Ibrahim Ismael na wengine watatu kuuawa Mombasa, Kenya, Oct. 3, 2013.

Waandamanaji katika mji wa Mombasa Kenya, wamechoma Kanisa moja na magurudumu ya magari Ijumaa baada ya watu wenye silaha kumpiga risasi Alhamis jioni na kumuuwa kiongozi mmoja maarufu wa ki-Islam na washirika wake watatu.

Ghasia zilizuka Ijumaa siku moja baada ya washambuliaji wasiofahamika kumfyatulia risasi Sheikh Ibrahim Rogo na washirika wake wakati wakisafiri ndani ya gari moja karibu na Mombasa.

Mashahidi wanasema polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na kuingia katika mapambano na vijana wa ki-islam katika kitongoji kimoja cha Mombasa.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema mtu mmoja alifyatuliwa risasi na kuuwawa wakati wa ghasia hizo.Sheikh Ibrahim Rogo alionekana kama mrithi wa Sheikh Aboud Rogo Mohammed, ambaye alihubiri kwenye msikiti huo huo mjini Mombasa na alishutumiwa kuwa na uhusiano na wanamgambo wa ki-Islam wa al-Shabab.

Ghasia zilizuka baada ya Rogo kuuwawa kwa kupigwa risasi Agosti 27 mwaka 2012 katika barabara hiyo hiyo ambayo pia Sheikh Ibrahim aliuwawa Ijumaa.