EU na Marekani wameelezea wasi wasi kwa maandamano ya upinzani huko Madagascar

Ghasia za kisiasa zinazoendelea huko Madagascar

Mahakama ya juu nchini humo wiki iliyopita iliamuru uchaguzi huo uahirishwe kwa wiki moja hadi Novemba 16, baada ya mgombea wa urais kujeruhiwa wakati wa moja ya maandamano ya kila siku ambayo yamelitikisa taifa lililopo kisiwa cha Bahari ya Hindi, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita

Umoja wa Ulaya na Marekani zimeelezea wasiwasi wao juu ya “matumizi mabaya ya nguvu” katika kutawanya maandamano ya upinzani nchini Madagascar, huku kukiwa na mvutano kabla ya uchaguzi wa rais.

Mahakama ya juu nchini humo wiki iliyopita iliamuru uchaguzi huo uahirishwe kwa wiki moja hadi Novemba 16, baada ya mgombea wa urais kujeruhiwa wakati wa moja ya maandamano ya kila siku ambayo yamelitikisa taifa lililopo kisiwa cha Bahari ya Hindi, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Katika taarifa ya pamoja, wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine saba na mashirika ya kimataifa ikiwemo Ufaransa, Ujerumani na Japan, wamesema wana wasiwasi kuhusu hali mbaya ya kisiasa huko Madagascar.

Walisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa kujieleza, ushirika na kukusanyika, na pia kutoa wito kwa pande zote “kuondoa kizuizi kilichopo” na kushiriki katika mazungumzo.

Hatua hiyo imekuja baada ya taarifa kutoka kwa kundi hilo mwezi uliopita ikisema kuwa inafuatilia uchaguzi huo kwa “uangalifu mkubwa”.