Mwanadiplomasia mkuu wa umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameeleza dhamira ya wazi ya EU na wanachama wake 28 kuendelea na utekelezaji kamili wa makubaliano ya nyuklia na Iran.
Mogherini mwakilishi wa masuala ya kigeni wa EU pamoja na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa EU walikutana kwa mazungumzo ya kawaida siku ya Jumatatu mjini Brussels na kujadili juu ya hali ya Libya na mkataba wa nuclear wa Iran.
Mwanadiplomasia huyo alikutana baadae na mawaziri wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo na kutoa msimamo huo wa kuunga mkono mkataba na kuionya Marekani dhidi ya kuongeza mzozo uliyopo.
Mazungumzo hayo yanafuatia onyo lililotolewa wiki iliyopita na Rais wa Iran, Hassan Rouhani ambaye alieleza kwamba Tehran itaweza kurudia kurutubisha uranium ya kiwango cha juu kama Umoja wa ulaya, China na Russia hazitaunda mpango wa kuzuia adhabu ya vikwazo vya Marekani kwa mabenki ya Iran na sekta za nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari baadae Mogherini alieleza kwamba mawaziri walimueleza Pompeo wasi wasi wao mkuu ulikuwa ni kudumisha amani na utekelezaji wa mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015.
Onyo la EU kuhusu kuongezeka hali ya mivutano limetolewa wakati Marekani ambayo ilijitoa kutoka mkataba wa kimataifa kupunguza nia ya iran kumiliki silaha za nyuklia imepeleka manuwari ya kubeba ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln na ndege nne za mashambulizi aina ya B-52 huko mashariki ya kati katika kujibu wasi wasi kwamba Iran huwenda inapanga shambulizi dhidi ya vituo vya Marekani.
Ratiba ya Pompeo kuelekea maeneo mengine inaendelea kama ilivyopangwa. Safari ya Pompeo inafanyika wiki chache kabla ya mkutano wa G-20 mjini Osaka nchini Japan na wote Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin wanatarajiwa kuhudhuria.