Ethiopia imefikia makubaliano kutumia bandari kuu eneo la Somaliland

Rais wa Somaliland, Muse Bihi Abdi (R) akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika mkataba wa kihistoria wa kutumia bandari. Picha imechukuliwa Addis Ababa, Ethiopia, Jan. 1, 2024.

Mkataba wa maelewano kati ya Ethiopia na Hargeisa ambao ni makao makuu ya serikali ya Somaliland ulitiwa saini na Abiy Ahmed na Muse Bihi Abdi

Ethiopia imefikia makubaliano ya kihistoria ya kutumia bandari kuu katika eneo la Somaliland lililojitenga na Somalia, wakati nchi hiyo isiyokuwa na bahari ikitafuta njia zaidi za bahari kwa ajili ya usafirishaji, maafisa wamesema Jumatatu.

Makubaliano hayo ya bandari ya Berbera ya Somaliland yanakuja miezi kadhaa baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kusema nchi yake ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, itatetea haki yake ya kupata fursa katika Bahari ya Sham, na kuzusha wasiwasi miongoni mwa majirani zake.

Katika pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden, Berbera inatoa kituo cha Kiafrika kwenye lango la Bahari ya Sham na kaskazini zaidi hadi mfereji wa Suez.

Mkataba wa maelewano (MOU) kati ya Ethiopia na Hargeisa, ambao ni makao makuu ya serikali ya Somaliland ulitiwa saini na Abiy na kiongozi wa Somaliland, Muse Bihi Abdi mjini Addis Ababa, ofisi ya Abiy imesema.

Mkataba huo utafungua njia ya kutambua utashi wa Ethiopia kupata fursa ya bahari na kupanua upatikanaji wake wa bandari, ofisi yake ilichapisha kwenye mtandao wa X.

Pia inaimarisha usalama wao, ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa, ilisema.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Abiy, Redwan Hussein amesema Ethiopia itakuwa na uwezo wa kupata kituo cha kijeshi kwa kukodi katika bahari ya Sham kama sehemu ya makubaliano hayo.

Hatua moja mbele katika mwelekeo sahihi kwa hili na vizazi vijavyo, Redwan alibandika ujumbe kwenye mtandao wa X.

Haikufahamika ni lini mkataba huo utaanza kutekelezwa.

Ethiopia ilikosa fursa ya pwani baada ya Eritrea kujitenga na nchi hiyo na kujitangazia uhuru mwaka 1993 kufuatia vita vya miongo mitatu.

Addis Ababa ilikuwa imedumisha upatikanaji wa bandari nchini Eritrea hadi nchi hizo mbili zilipoingia vitani kati ya mwaka 1998 na 2000, na tangu wakati huo Ethiopia iliendeleza biashara yake kupitia Djibouti.