Kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro, anasema taifa hilo la visiwa vya Carribean litashirikiana “kwa nia njema” na Marekani katika kupambana dhidi ya ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi.
Castro aliandika ujumbe huo kwa televisheni ya kitaifa ya Cuba Jumamosi. Castro mwenye umri wa miaka 88 alisema ushirikiano huo ni kwa maslahi ya “amani duniani,”na wala sio juhudi za kutafuta suluhu la maswala baina ya Marekani na Cuba.
Mtangazaji wa televisheni ya Cuba alisoma ujumbe wa maandishi wa bwana Castro hewani.
Siku ya Ijumaa waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisifu juhudi za Cuba kufuatia mlipuko wa Ebola, akisema kuwa “Cuba,nchi ya watu milioni 11na imepeleka wataalam wa afya 165, na ina mpango wa kupeleka wengine takriban 300” kuisaidia nchi za Afrika Magharibi zilizoathiriwa zaidi.
Cuba ina historia ya kupeleka madaktari wake kote duniani inapotokea dharura.