Chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza cha Labour kinasema kuwa kama kitashinda madaraka kitamteuwa “Kamishna wa rushwa katika masuala ya COVID” ili kujaribu kurejeshwa kwa mabilioni yaliyopotea kwa udanganyifu wa matumizi mabaya wakati wa janga hilo.
Msemaji wa kitengo cha uchumi katika chama cha Labour Rachel Reeves anatarajiwa kuelezea mpango huo katika hotuba yake ya Jumatatu kwenye mkutano wa kila mwaka wa chama hicho. Anasema kamishna atawaleta pamoja maafisa wa kodi, wachunguzi wanaofuatilia ubadhirifu na maafisa wa polisi kufuatilia takriban dola bilioni 8.8 fedha za umma zilizopotea ambazo zilitumika kwa misaada na mikataba inayohusiana na COVID-19.
Kama ilivyo katika nchi nyingi, Uingereza ililazimika kuweka kando sheria za kawaida wakati ikiharakisha kununua vifaa muhimu na kuimarisha maisha ya watu wakati wa janga la virusi vya corona.
Reeves ameiambia BBC kuwa serikali ya ki-Conservative “ilitia aibu” na kiwango cha hasara na kutofanya chochote katika kurejesha fedha hizo. Uchunguzi wa umma wa miaka mingi uliangalia namna Uingereza ilivyoshughulikia janga hilo ambalo lilipelekea vifo vya zaidi ya watu 200,000 nchini humo.