Kundi la familia zilizopoteza jamaa zao wakati Iran ilipotungua ndege ya abiria ya Ukraine mwaka 2020 wameiambia VOA kuwa mataifa manne ambayo yalianzisha hatua za kisheria za kimataifa katika kesi hiyo mwezi huu hayajaunga mkono ombi lao la uchunguzi tofauti wa kimataifa.
Chama cha familia za wahanga wa Ndege nambari PS752 mwezi Septemba kiliomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC, ofisi ya mwendesha mashtaka kupanua uchunguzi wake wa madai ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine ili kujumuisha shambulio la makombora la Iran lililoiangusha ndege ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine ilipopaa kutoka Tehran Januari 8, 2020.
Shambulio hilo la kombora liliwauwa abiria wote 176 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wengi wao wakiwa raia wa Iran na Canada waliokuwa wakiruka kuelekea Canada kupitia Kyiv. Iran inasema kuwa vikosi vyake vilichanganya ndege hiyo na kombora la Marekani.