Caroline Kennedy akaribishwa Japan

Balozi mpya wa Marekani nchini Japan Caroline Kennedy akiwasili Tokyo, Nov. 19, 2013.

Maelfu ya watu walipanga foleni katika mitaa ya Tokyo Jumanne kumkaribisha Caroline Kennedy ambaye atakuwa balozi mpya wa Marekani nchini humo.

Bi.Kennedy mwenye umri wa miaka 55 alitabasamu na kuwapungia mikono wananchi hao wa Japan akiwa amebebwa kwa njia ya kitamaduni kabisa na farasi wa kifahari waliopambwa na kuelekea kasri ambako aliwasilisha hati zake kwa Emperor Akihito katika sherehe zilizoandaliwa kwa heshima yake.

Na ingawa ni kawaida kwa mabalozi wanaopelekwa Japan kukutana na Emperor Akihito, sherehe za kumkaribisha Caroline Kennedy zilikuwa za aina yake na ziliandaliwa kwa heshima kuu na kupeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni za Japan.

Kennedy ni mtoto pekee aliye hai katika familia ya rais wa zamani wa Marekani J.F. Kennedy ambaye sherehe za miaka 50 za kuadhimisha kifo chake zinafanyika wiki hii.

Caroline Kennedy ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa na Marekani kama balozi wake nchini Japan.