Blinken Jumapili azungumza moja kwa moja na mwenzake wa Russia Sergey Lavrov kwa njia ya simu

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kwamba waziri wake Antony Blinken Jumapili amezungumza kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya kigeni wa Russia Sergey Lavrov.

Blinken aliomba kuachiliwa mara moja kwa mwandishi habari wa gazeti la Wall Street Journal Evan Gershkovich, ambaye Russia inatuhumu kuchunguza taarifa muhimu. Naibu msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani hata hivyo hakutaja jina la mwanahabari huyo wakati wa kutoa taarifa.

Majibu ya Lavrov kwa Blinken yalikuwa kwamba hatma ya Gershkovich itaamuliwa na mahakama ya Russia, wakati akiongeza kuwa haikubaliki kwa Washington kuingiza siasa kwenye kesi hiyo. Lavrov amesema kwamba kuna ushahidi wa kutosha dhidi yake ,ingawa Russia haijaufichua.

Taarifa imeongeza kusema kwamba Blinken pia aliomba kuachiliwa kwa raia wa Marekani Paul Whelam ambaye amekuwa kizuizini kwa siku 1,553 baada ya kupewa hukumu ya miaka 16 na mahakama ya Russia kwa tuhuma za ujasusi.