Blinken azuru Jordan baada ya kuondoka Israel kwa mazungumzo kuhusu vita vya Israel na Hamas

Waziri wa mabo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na waziri mkuu wa Qatar Mohammed bin Adulrahman al Thani, Amman, Jordan. Novemba 4, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken yuko Amman, Jordan, kufuatia ziara yake nchini Israel kwa mazungumzo kuhusu vita vya Israel na Hamas.

Akiwa Amman, Blinken amekutana maafisa wa Jordan, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Qatar, pamoja na katibu mkuu wa kamati ya utendaji la Palestine Liberation Organization. Wamekuwa wakikutana kupanga mipango ya kumaliza mzozo wa kibinadamu huko Gaza na vita kati ya Israel na Hamas.

Blinken pia amekutana Jumamosi na wazri mkuu wa muda wa Lebanon, Najib Mikati. Kabla ya ziara ya Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Jordan Ayman Safadi alisema katika taarifa yake kwamba Israel lazima imalize vita huko Gaza, ambako amesema inatenda uhalifu wa kivita kwa kuwapiga mabomu raia na kulizingira eneo hilo.

Ijumaa, Blinken alisema kwamba kuzuia kusambaa na kuenea kwa mzozo huo wa takriban mwezi mzima kati ya Israel na Hamas, ilikuwa ni kipaumbele chake baada ya kukutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, na baraza la mawaziri la Israel linaolhusika na vita mjini Tel Aviv.

Baada ya kikao chao Blinken aliwaeleza wana habari kwamba kuna hatua ambazo lazima zichukuliwe kuhakikisha kuwa shambulizi kama la Hamas la Oktoba 7 kamwe halitokei tena, na kuhakikisha “siku njema ya kesho” kwa watu wa Israel na Palestina.

Licha ya kuwaamuru raia kuondoka maeneo ya kaskazini mwa Gaza, jeshi la Israel limeendelea kupiga mabomu upande wa kusini wa ukanda huo pia. Mamlaka za Hamas na hospitali ya al-Shifa zimekanusha kuwa eneo hilo linatumiwa kama kambi ya wanamgambo wapiganaji.

Katika majibu yake, Netanyahu amesema, “Tunaendelea na operesheni zetu, na Israel inapinga sitisho la muda la mpigano ambalo halijumuishi kuachiliwa kwa mateka wetu.” Marekani imelitaja kundi la Hamas ni la kigaidi ambalo limechukua mateka 230 na kuua watu 1,400 katika shambulizi lao.

Maelfu ya wapalestina wameachwa bila ya makazi kutokana na mashambulizi ya Israel ikiwa ni majibu kwa shambulizi la kigaidi la Hamas. Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema siku ya Ijumaa kuwa idadi ya vifo katika eneo hilo imefikia 9,250, Umoja wa Mataifa imesema.