Blinken akamilisha mazungumzo na Mfalme wa Jordan kuhusiana na vita vya Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiondoka Marekani kuelekea Mashariki ya Kati mwishoni mwa wiki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye yupo kwenye ziara ya siku kadhaa Mashariki ya Kati Jumapili amekutana na mfalme wa Jordan Adullah wa pili.

Kwenye kikao hicho pia alikuwemo waziri wake wa mambo ya kigeni Ayman Safadi, wakati Blinken pia akitembelea ghala la shirika la chakula duniani, WFP nchini humo, ambako malori ya misaada kuelekea Gaza hupakia mizigo.

Jordan ndilo taifa la pili kutembelewa na Blinken baada ya kuondoka Uturuki Jumamosi, ikiwa ziara yake ya nne ya Mashariki ya Kati tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israel na Gaza. Jordan na mataifa mengine ya Kiarabu wamekuwa wakiitisha sitisho la mara moja la mapigano hayo, yaliozuka Okotoba, lakini Israel imekaidi mwito huo.

"Uturuki ipo tayari kutumia ushawishi wake pamoja na mataifa washirika ya Mashariki ya Kati, kujaribu kuzuia kuenea kwa mzozo wa Gaza," Blinken ameambia wanahabari Jumamosi muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza.