Rais wa Marekani Joe Biden Ijumaa ametembelea mji wa Rolling Fork Mississippi, ulioathiriwa vibaya na kimbunga licha ya tishio la vimbunga zaidi kupiga sehemu kubwa ya Magharibi Kati na Kusini mwa Marekani.
Kimbunga cha wiki iliyopita kiliharibu karibu nyumba 300 na biashara kwenye mji huo pamoja na mwingine wa karibu wa Silver City, na kuacha vifusi vilivyojaa mawe, mbao na vyuma vilivyokunjika.
Idadi ya vifo kutokana na kimbunga hicho imefikia 21 wakati mtu mmoja akiripotiwa kufa kwenye jimbo jirani la Alabama. Biden anatarajiwa kutangaza kwamba serikali itagharamia shughuli za dharura jimboni humo kwa siku 30 zijazo ikiwemo mishahara ya waokozi pamoja na wale wanaoondoa vifusi.
Biden na mke wake Jill Biden watajionea wenyewe hasara iliyotokea pamoja na kukutana moja kwa moja na wamiliki wa nyumba zilizoharibika.