Biden atangaza msaada wa dozi milioni 17 zaidi za Chanjo za Covid-19 kwa Afrika

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akutana na Rais wa Marekani Joe Biden katika Ikulu mjini Washington DC. Alhamisi Oktoba 14, 2021.

Rais Joe Biden alimwambia Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Alhamisi kwamba Marekani itatoa msaada wa mara moja wa dozi zaidi ya milioni 17 za chanjo ya Johnson & Johnson kwa Umoja wa Afrika.

Biden alitangaza hayo wakati wa mkutano na Kenyatta kwenye afisi yake ya Ikulu mjini Washington DC, ambao pia ulijadili ushirikiano katika masuala mbalimbali.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Marekani kutoa msaada wa chanjo za Covid-19 kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, baada ya kutangaza hatua ya kutoa takriban dozi milioni hamsini mwezi Julai mwaka huu.

Tayari chanjo hizo zimetumwa kwa nchi mbalimbali, ikiwemo Kenya ambayo imepokea dozi milioni 2.5 kutoka kwa mpango huo.

"Tunatumai kuwa msaada huu utasaidia nchi za AU katika programu za chanjo kusaidia watu kupata chanjo hizo," Biden alisema.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza wa Biden akiwa rais, na kiongozi wa Kiafrika.

Rais huyo alisema kwamba Kenya ni mshirika muhimu wa Marekani na amewajibika vilivyo kama kiongozi wa kieneo katika nyanja ya amani na usalama.

“Kenya inashikilia urais unaozunguka wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu. Ahsante kwa kukubali tuendelee kuwepo,” Biden alisema kwa utani.

Kenyatta alimshukuru Biden kwa kutangaza msaada huo wa chanjo akisema kwamba Afrika imesalia nyuma mno katika utoaji wa chanjo kwa watu wake.

“Tunathamini ushirikiano wetu na Marekani katika masuala kama vile kupambana na ugaidi na mabadiliko ya hali ya hewa. Nchi yetu, na bara la Afrika kwa jumla linachangia kiasi kidogo cha uchafuzi wa mazingira lakini linalipa gharama kubwa. Sasa Marekani imerejea kwenye mkataba wa Paris, tunaukaribisha uongozi wako katika hili," alisema Kenyatta.

Marekani na Kenya kwa muda mrefu zimeshirikiana katika nyanja mbalimbalimi zikiwemo biashara na usalama, pamoja na kupambana na ugaidi.

Jumuiya ya Afrika, ambayo ina nchi wanachama 55 na idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.3, katika siku za nyuma imewatuhumu watengenezaji wa chanjo kwa kutozingatia haki katika utoaji wa chanjo hizo kwa nchi zinazohitaji.

Kufikia wiki iliyopita, ni asilimia 4.5 tu ya Waafrika walikuwa wamepewa chanjo kamili dhidi ya COVID-19, kulingana na afisa mkuu wa afya wa umma barani humo John Nkengasong.

White House ilisema Mkutano huo ni mwendelezo wa ahadi ya Biden, aliyoitoa wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Kenyatta mwezi Februari mwaka huu, kuhusu ushirikiano na bara la Afrika, "katika hali ya kuheshimiana na usawa."

Kati ya mengine pia, Biden na Kenyatta walizungumza kuhusu haja ya uwazi, na uwajibikaji, wa mifumo ya fedha, ya ndani ya nchi, na ya kimataifa.

Viongozi hao wawili pia walijadili juhudi za kulinda demokrasia, haki za binadamu, kuimarisha amani na usalama, wakati ambapo Marekani inatafakari kuiwekea vikwazo Zaidi serikali ya Ethiopia.

Wawili hao pia wanazunguzma kuhusu juhudi za kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Profesa Fubert Namwamba, Mchambuzi wa masuala ya Siasa za kimataifa, Alhamisi aliiambaia VOA kwamba suala la chanjo kwa bara la Afrika halingeepukika kwenye mkutano huo.

"Limekuwa ni suala muhimu kwa sababu taswira imejitokea kwamba wakati nchi hizo zina chanjo za ziada, nchi zinazoendelea zinazidi kukumbwa na changamoto ya ukosefu wa chanjo," alisema, akizungumza katika mahojiano kwenye kipindi cha televisheni cha Duniani Leo.