Kikundi hicho kimetangaza kinasitisha operesheni zote za kijeshi dhidi ya vikosi vya Marekani katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Joe Biden Jumanne alisema ameamua kuchukua hatua za kijeshi kujibu shambulizi lililofanywa katika kambi ya jeshi ya Marekani nchini Jordan karibu na mpaka wa Iraq na Syria lililouwa wanajeshi watatu wa Marekani na kujeruhi wengine zaidi ya 40.
Siyo Biden wala maafisa wake waliotoa maelezo ya kina. Lakini akizungumza na waandishi katika ndege ya Air Force One, msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa John Kirby alisema lengo ni kuhakikisha Marekani inapunguza uwezo wa kivita wa makundi haya kuweza kuyashambulia majeshi ya Marekani na vifaa vyake, huku ikipeleka ujumbe kwa wanaowaunga mkono” kwa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi wa Jamhuri ya Kiislam.
“Rais atafanya kila anachoweza kuwalinda wanajeshi wetu na vifaa vyetu na kuangalia usalama wa kitaifa … maslahi katika eneo,” alisema, akiongeza kuwa amri aliyoitoa Biden itakuwa “na utaratibu wa ngazi kadhaa” ikikusanya “uwezekano wa hatua mbalimbali kadhaa.”
Mashambulizi ya Jumapili katika kambi ya kijeshi ya Marekani huko Jordan yaliuwa wanajeshi wetu kwa mara ya kwanza katika Mashariki ya Kati tangu vita vya Israeli na Hamas kuzuka huko Gaza Oktoba 7.
Kikundi kinacho simamia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, Islamic Resistance huko Iraq, kimedai kuhusika na shambulizi hilo. Wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema shambulizi la droni hiyo linayo “alama” ya wanamgambo wa Kataib Hezbollah, wanaoungwa mkono na Iran, japokuwa Marekani haijatoa kauli ya mwisho juu ya nani ni wa kuwajibishwa.
Siku ya Jumanne, Kataib Hezbollah ilisema kusitisha kwa operesheni za kivita dhidi ya majeshi ya Marekani katika eneo kumefanyika “ ili kuepusha fedheha kwa serikali ya Iraqi.”
Tutaendelea kuwalinda watu wetu huko Gaza kwa njia nyingine,” Katibu Mkuu wa Kikundi hicho Abu Hussein al- Hamidawi alisema katika taarifa iliyotolewa na kikundi hicho kupitia mtandao wa Telegram.
Kataib Hezbollah haikutangaza kitu chochote kuhusu tishio la kuwepo kisasi cha Marekani katika kulipiza kisasi. Lakini tamko hili siyo kwamba limesadifu bila ya kukusudia, alisema Mathew Kroenig, mkurugenzi wa ngazi ya juu wa kituo cha mikakati cha Atlantic Council Scrowcroft.
“Ni suala jepesi kabisa: Wakati Marekani ikiweka hatua mbalimbali mbadala za kijeshi za kwelikweli mezani, mahasimu wake wananyweya,” aliiambia VOA.
Hatua ya Kataib Hezbollah kusitisha mashambulizi siyo rahisi kubadilisha msimamo wa Washington wa kupanga kulipiza kisasi. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Meja Jenerali Pat Ryder amewaambia waandishi wa habari Jumanne kuwa “vitendo vinaonekana zaidi kuliko maneno,” na kuapa “kuwepo malipizo.” – VOA, AP and Reuters
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP na Reuters.