Biashara kati ya China na Russia imeripotiwa kufikia zaidi ya dola bilioni 240, kulingana na takwimu za idara ya ushuru, kiwango ambacho kimepita dola bilioni 200 zilizokisiwa na mataifa hayo wakati wa kikao cha pamoja mwaka uliopita.
Kiwango hicho ndicho kikubwa zaidi kati ya mataifa hayo ambayo uhusiano wao unaonekana kushamiri kiuchumi na kisiasa tangu Moscow ilipofanya uvamizi wa Ukraine mwaka 2022. Beijing imekuwa ikikosolewa na mataifa ya magharibi kutokana na msimamo wake kuhusu uvamizi wa Ukraine, licha ya kusisitiza kwamba haiungi mkono upande wowote.
Hata hivyo imejiepusha kuikosoa Russia moja kwa moja. Kulingana na takwimu za Ijumaa, biashara kati ya mataifa hayo mawili imeongezeka kwa asilimia 26.3, wakati biashara kati ya Marekani na China ikiripotiwa kushuka kwa asilimia 11.6 kuanzia 2022.