Mwanariadha raia wa Uganda Benjamin Kiplagat amekutwa amekufa nchini Kenya, polisi wamesema Jumapili, huku vyombo vya habari nchini humo vikiripoti kuwa alichomwa kisu hadi kufa.
Kiplagat mzaliwa wa Kenya mwenye umri wa miaka 34, alikuwa ameiwakilisha Uganda kimataifa katika mbio za mita 3,000 za kuruka viunzi ikiwa ni pamoja katika michezo kadhaa ya Olimpiki na mashindano ya dunia.
Mwili wake ulipatikana ndani ya gari Jumamosi usiku kwenye viunga vya Rift Valley katika mji wa Eldoret ambao ni makaazi kwa wanariadha wengi wanaopatiwa mafunzo katika eneo nyanda za juu.
Uchunguzi umeanzishwa na maafisa wa polisi wako katika eneo wakiangazia chanzo kilichopelekea kifo chake, kamanda wa polisi Stephen Okal aliwaambia waandishi wa habari huko Eldoret.
Alisema mwili wa Kiplagat ulikuwa na jeraha kubwa la kisu shingoni mwake, akieleza kuwa alichomwa kisu.
Gazeti la Daily Monitor la Uganda na vyombo vingine vya habari nchini Kenya, vimesema kuwa alichomwa kisu hadi kufa.
Wanariadha duniani wameshtushwa na kuhuzunishwa kusikia kifo cha Benjamin Kiplagat, shirikisho la kimataifa la riadha duniani lilisema katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa X zamani ukiitwa Twitter.
“Tunatuma salamu za rambirambi kwa marafiki zake, familia, wachezaji wenzake na wanariadha wenzake. Hisia zetu ziko pamoja nao katika wakati huu mgumu.”
Peter Ogwang, Waziri wa michezo nchini Uganda, alielezea hisia kama hizo kwenye mtandao wa X.
“Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia yake, Waganda na Afrika Mashariki kwa kumpoteza mwanariadha huyo chipukizi ambaye mara kadhaa ametuwakilisha katika medani ya kimataifa”, alisema.
Taarifa za vyombo vya habari zinasema Kiplagat alikuwa akifanya mazoezi katika eneo la Eldoret kabla ya kwenda Uganda kushiriki mashindano ya riadha.
Kiplagat, ambaye kazi yake ya kukimbia ilidumu kwa miaka 18, alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 3,000 katika mashindano ya dunia ya vijana na shaba katika mashindano ya Afrika mwaka 2012.
Alishiriki nusu fainali ya mashindano hayo katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 mjini London na pia alishinda katika mashindano ya Rio mwaka 2016.