Baadhi ya Mashirika ya Kimataifa yasitisha utoaji wa misaada kutokana na kuongezeka kwa ghasia Sudan

Watu waliokoseshwa makazi wakusanya bidhaa zao baada ya kuondoka Wad Madani, mji mkuu wa jimbo la al-Jazirah state, Desemba 18.2023

Kuenea kwa mapigano kusini mashariki mwa Sudan kumeyalazimisha  mashirika ya misaada ya kibinadamu kusitisha kwa muda operesheni zao kwenye baadhi ya maeneo, wakati UNICEF ikielezea wasi wasi wake kuhusu mamilioni ya watoto walio hatarini kutokana na ghasia zinazosambaa.

UNICEF imesema Alhamisi kwamba takriban watoto 150,000 katika wiki moja iliyopita wamelazimika kuondoka katika jimbo la Jazeera lililopo kusini mashariki mwa mjini mkuu Khartoum. Hayo yamejiri wakati kundi la kijeshi la Rapid Support Forces, RSF likitangaza limechukua udhibiti wa wa Wad Medani, kutoka mikononi mwa jeshi.

UNICEF imesema kwamba Wad Medani ulikuwa muhimu kwa misaada kutokana na kuwa maelfu ya watoto waliokuwa wamekimbia kutoka sehemu nyingine za Sudan, walikuwa wamechukua hifadhi huko. Shirika la mpango wa chakula duniani WFP, pia limetangaza kwamba operesheni zake zimeathiriwa na kuenea kwa mapigano, na hivyo kutangaza kusitisha kwa muda upelekaji wa misaada ya chakula kwenye baadhi ya maeneo ya Jazeera.

Mwakilishi wa WFP na mkurugenzi wa kanda Eddie Rowe amesema katika taarifa yake, “Usalama wa wafanyakazi ni muhimu sana na lazima kuwe uhakikisho huo bila ya kujali hali iliyopo.”