Viongozi kadhaa kwenye serikali ya Ukraine Jumanne wametangaza kujiuzulu kwa kile ambacho rais Volodymyr Zelenskyy ametaja kuwa baadhi ya mabadiliko katika serikali yake.
Naibu waziri wa ulinzi Viacheslav Shapovalov ambaye alikuwa akisimamia maswala ya kiufundi katika vikosi vya Ukraine amejiuzulu wadhifa wake akielezea tuhuma za sakata la ununuzi wa chakula, kashfa ambayo ameikanusha.
Naibu mwendesha mashtaka mkuu jenerali Olesiy Symonenko pamoja na naibu mkuu wa ofisi ya rais Kyrylo Tymoshenko pia wamejiuzulu bila ya kutoa sababu za kuondoka kwao.
Katika hotuba yake kwa taifa Jumatatu jioni, Zelenskyy amesema kwamba tayari kuna maamuzi binafsi yaliyofanyika, baadhi yakifanyika Jumatatu mengine Jumanne na katika siku zijazo, kuhusiana na maafisa mbali mbali katika ngazi za uwaziri na miundo ya serikali kuu, pamoja na katika mikoa na kwenye vikosi vya usalama.